Mpeni Bwana, enyi mashujaa, mpeni Bwana utukufu na nguvu.Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake; mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake.Sauti ya Bwana iko juu ya maji; Mungu wa utukufu hupiga radi, Bwana hupiga radi juu ya maji makuu.Sauti ya Bwana ina nguvu; sauti ya Bwana ni tukufu.Sauti ya Bwana huvunja mierezi; Bwana huvunja vipande vipande mierezi ya Lebanoni.Hufanya Lebanoni irukaruke kama ndama, Sirioni urukaruke kama mwana nyati.Sauti ya Bwana hupiga kwa miali ya umeme wa radi.Sauti ya Bwana hutikisa jangwa; Bwana hutikisa Jangwa la Kadeshi.Sauti ya Bwana huzalisha ayala, na huuacha msitu wazi. Hekaluni mwake wote wasema, “Utukufu!”Bwana huketi akiwa ametawazwa juu ya gharika; Bwana ametawazwa kuwa Mfalme milele.Bwana huwapa watu wake nguvu; Bwana huwabariki watu wake kwa kuwapa amani.